Friday, 15 April 2016

Phiri:Wachezaji wangu wa viwango




Kocha Mkuu wa Mbeya  City Fc  Mmalawi Kinnah Phiri amesema  sasa ana uhakika  kuwa nyota wake wako kwenye kiwango kizuri  kufuatia  matokeo ya  ushindi wa jumla ya mabao 5  kwenye michezo miwili  iliyopita  kwenye  mfululizo  wa mechi za  Ligi Kuu ya Soka  Tanzania Bara inayoelekea  ukingoni hivi sasa. 
Phiri15
Kocha Kinnah Phiri
Phiri ameayasema hayo leo wakati akizungumza na mtandao wa Mbeya City fc.Com na kuweka wazi kuwa  ushindi wa 4-0 dhidi ya Coastal Union na  ule wa 1-0 dhidi ya Mgambo JKT mwishoni mwa juma lililopita umempa  imani kubwa kuwa wachezaji wake sasa  wameanza kuielewa vyema  falsafa yake hasa kwa kuweza kufanikisha ushindi bila  kuruhusu kufungwa bao katika michezo hiyo miwili.
"Tulianza  kucheza  kwa  mchezo wa kawaida  sasa  tumeongeza, tunacheza kwa spidi kubwa wachezaji wangu sasa  wanajiamini kwa kiwango kikubwa, tumefunga bao 5 bila kuruhusu kufungwa bao lolote, ni uhakika tosha kuwa kikosi changu sasa  kiko imara kwenye ulinzi," amesema na kuongeza.
"Pia  kiko vizuri kwenye ufungaji, kwa sasa  tuko kwenye mipango  mizito  kuhusina na mchezo ujao."
Kocha huyo aliyewahi  kuifundisha Timu ya Taifa ya Malawi alisema kuwa  mara baada ya kurejea  kutoka  jijini Tanga kwenye mchezo dhidi ya Mgambo JKT  alitoa siku chache za mapumziko kwa wachezaji wake na kuwataka  kujiandaa kwa mazoezi yatakayoanza  siku ya jumatatu tayari kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopangwa  kuchezwa  mwishoni  mwa mwezi huu.


"Baada ya kutoka Tanga, nilitoa mapumziko ya siku saba, vijana watarejea  jumatatu tayari kwa mazoezi  kabla ya kuivaa Mtibwa, nina  imani siku saba  zitatosha  kuwaweka sawa kwa ajili ya mchezo huo," amesema.
"Sifahamu sana  kuhusu timu hiyo ya Morogoro, kwenye ratiba  inaonyesha watacheza kesho  ninaweza kufika  kuwaona au  nitatumia  muda kuangalia mchezo wao kwenye TV, nataka kujua baadhi ya mambo muhimu ili nijiandae  vizuri kuweza kupata ushindi," amesem.

No comments: