Friday 1 August 2014

Ngoma nzito leo CCM vs Ukawa

Kete ya mwisho ya kuamua iwapo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watarejea katika Bunge la Katiba au la itachezwa leo katika kikao cha maridhiano baina ya umoja huo na CCM, chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.


Kikao hicho kinafanyika siku nne kabla Bunge hilo kuendelea na vikao vyake Jumanne ijayo licha ya msimamo wa Ukawa wa kuendelea kuvisusia.

Kikao hicho kinachovikutanisha vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na CCM ni cha mwisho baada ya kile cha kwanza kilichofanyika wiki moja iliyopita kumalizika bila mwafaka wowote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa na wenyeviti wenzake, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hadi jana msimamo wao ni kutohudhuria vikao vya Bunge hilo labda ikitokea miujiza katika kikao cha leo.

Mbowe alisema ni miujiza kwa sababu kwa madai ya Ukawa, ni lazima mjadala huo ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi na kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka CCM, kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha ambayo si rahisi wenzao kuyakubali.

Moja ya ajenda ya kikao hicho ambacho leo kitakuwa na wajumbe 20 kutoka kila chama, ni kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni ili kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

Ukawa walisusia vikao vya Bunge la Katiba hilo Aprili 16 wakipinga kubadilishwa Rasimu ya Katiba na wajumbe wa CCM kwa maelezo kuwa ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Mbowe alisema ni jambo la kushangaza kuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta wakitoa kauli za kuwashutumu Ukawa wakati wakijua wazi kuwa kuna mazungumzo kati ya vyama vya siasa na Jaji Mutungi vinaendelea.

Juzi pia, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), liliisihi Ukawa kurudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini likasema mjadala huo uzingatie Rasimu ya Katiba.

“Hata viongozi wa dini nao wametoa matamko wakitaka Ukawa turejee bungeni, tunashukuru maoni yao. Ila wanatakiwa kujua sababu zilizotufanya mpaka tukasusia. Wanatakiwa kuwaonya CCM wanaokwenda kinyume na mchakato huo,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Wakati tupo katika mazungumzo, Sitta anaanzisha kikao chake na kutoa tamko kuwa Bunge litaendelea wakati akijua Ukawa wapo katika kikao pamoja na viongozi wa chama chake cha CCM. Kauli hizi zinazokosa umoja zinaonyesha Serikali na timu nzima haiko tayari kutafuta mwafaka wa suala hili.”

No comments: