Saturday, 5 March 2016

TFF: Atuhusiki wala hatujatoa kibali cha michezo ya Betting


SHIRIKISHO la  Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema halihusiki na halijawahi kutoa kibali chochote cha kuhusisha  mashindano yake na michezo ya kubahatisha.
 Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto ameyasema hayo leo katika ofisi za TFF zilizopo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa Shirikisho limepokea kwa mshtuko taarifa za kuwepo makundi ya watu na makampuni wanaochezesha michezo ya kubahatisha inayohusu mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na kusimamiwa na TFF (betting).
“TFF inauthibitishia umma wa watanzania kuwa Shirikisho halihusiki wala halijawahi kutoa kibali chochote cha kuhusisha mashindano yake na michezo ya kubahatisha,” amesema Kizuguto.
 Moja ya jengo linalotoa huduma za mchezo wa kubahatisha (Betting)
Kizuguto amefafanua hatua zilizochukuliwa na TFF baada ya kubaini hilo, ikiwa ni pamoja na kuwaandikia barua wahusika ambao ni makampuni ya nje.
“Kwa kuwa baadhi ya wahusika wa matendo hayo ni makampuni ya nje ya nchi hivyo TFF imechukua hatua zifuatazo:
1.TFF imeandika barua kwenye Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa ili kupata mwongozo wa kisera na kisheria kuhusu haki na majukumu ya Shirika hilo  katika kudhibiti na kusimamia  jambo hilo.
2.TFF imeandika barua kwa kitengo cha sheria cha FIFA ili kupata mwongozo na ushauri wa namna ya kudhibiti makampuni ya nje yanayoshiriki mchezo huu.
TFF inawaomba wadau wa mpira wa miguu na washiriki wa michezo ya kubahatisha wajiepushe kushiriki michezo ya kubahatisha inayohushu michezo yote inayoandaliwa na TFF,” amesema Kizuguto.

No comments: