Saturday 5 March 2016

Jamii Media yaitaka Mahakama Kuu kurekebisha vifungu vya sheria ya mtandao


Na Regina Mkonde
KAMPUNI ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com imefungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kesi Na. 9 ya mwaka 2016 la kuitaka Mahakama kurekebisha sheria ya makosa ya mtandao vifungu Na. 32 na 34
Hatua hiyo imefikiwa baada ya miezi mitatu iliyopita Kampuni hiyo kupata mashinikizo kutoka kwa Jeshi la Polisi (kwa njia ya barua rasmi) kuitaka itoe taarifa za baadhi ya wateja wanaoonekana kutoa taarifa zinazoibua ufisadi na ukwepaji kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa shauri hilo katika Mahakama Kuu iliyopo jijini dar es Salaam jana, Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media amesema kuna ulazima wa vifungu hivyo kuangaliwa upya kwa kuwa vinapelekea kuvunjwa kwa haki ya kulindwa uhuru wa utoaji maoni.
“Baada ya kupata mashinikizo takribani manne yanayoashiria kuwa haki ya watanzania watumiao mitandao ya kijamii hasa mtandao wa Jamii Forums inavunjwa, Jamii media imeshauriana na Wanasheria wake na kuona ni wakati wa kulinda haki ya wananchi,” alisema Melo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media Maxence Melo (Kushoto) akiwa kati ya moja ya mikutano na waandishi wa habari.

Melo alisema kuwa, lazima watailinda haki ya wananchi ya kupata taarifa na kulindwa kwa uhuru wao wa maoni na kujieleza inayolindwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ibara ya 18.
 “JamiiForums katika kuhakikisha inasimamia usiri(Privacy) wa wateja wake imekuwa ikihoji mashinikizo hayo yanazingatia sheria gani na kutaka kujua vifungu gani vya sheria ambavyo wadau hao wa mtandao wamevivunja,” alisema.
Alisema, hawakuwepewa majibu yoyote na Jeshi la Polisi badala yake kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama hawatatoa ushirkiano kwa Jeshi hilo.

Benedict Alex, Wakili wa Kampuni ya Victory Attoneys anasimamia Shauri hilo, alisema kuwa vifungu hivyo vinakinzana na Katiba ya nchi na kwamba ili iende sambamba na katiba haina budi kubadilishwa.

No comments: