Wednesday, 16 July 2014

Kama tutajilinda inawezekana ukimwi kutokomea



Ukimwi mwisho mwaka 2030 inawezekana
Virusi vya ukimwi
Ifikapo mwaka 2030 kuna uwezekano wa kutokuwepo kwa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi(V.V.U) kauli hii ilitolewa na wataalamu kutoka shirika la umoja wa mataifa linaloshughurikia maswala ya Ukimwi.
Wataalamu hao walidai kuwa takwimu inaonyesha kuna udhibiti mkubwa wa maambukizo mapya ya virusi vya ukimwi na idadi ya watu wanaofariki kutokana na virusi hivyo imezidi kupungua tofauti na hapo awali,licha ya hivyo inahitajika nguvu ya ziada ili kupambana na ugonjwa huo.
Wataalamu hao walisema kuwa endapo matumizi ya dawa za kulevya yatakomeshwa,kutumia vifaa salama wakati wa kutahiri,kutumia kinga,pamoja na kufuata masharti ya dawa kwa walioathirika itaweza saidia kutokomeza janga hili miaka kadhaa ijayo.
Dawa za kurefusha na kupunguza makali ya virusi vya ukimwi.
Nchi nyingi sana zimejikuta zikiingia katika janga hili kutokana na baadhi ya mambo ambayo kama yangekomeshwa Ukimwi usingeweza kuwaathiri na kuua watu wengi mpaka sasa,elimu inayoendelewa kutolewa juu ya V.V.U imechangia kupunguza  maambukizi mapya na vifo vya mara kwa mara.
Kutokana na jitihada zinazofanywa na wataalam mbali mbali zimeleta mabadiliko makubwa tofauti na miaka 5 iliyopita,licha ya hivyo waathirika wa miaka 25 iliyopita walikuwa na asilimia chache ya kuishi tofauti na waathirika wa miaka ya hivi karibu,hii inaonyesha jinsi dawa za kurefusha maisha na kupunguza makali ya virusi vya ukimwi zinavyo fanya kazi.
Hapo awali watu wengi walikuwa waoga kuangalia afya kwa kuhofia kutengwa na kunyanyapaliwa endapo watagundulika ni waathirika wa virusi vya ukimwi,pia watu wengi waliweka dhana kwamba muathirika ni marehemu mtarajiwa hivyo basi baadhi ya waathirika wenye roho mbaya walithubutu kuwaambukiza kwa makusudi wengine ili wafe wengi.
Lakini baada ya dawa na elimu kutolewa watu wengi wamekuwa na uthubutu wa kuangalia afya zao huku wengi wao wakikumbuka kinga na kuacha kupima watu kwa macho.
Hapo awali watu wengi walikuwa wakimtafsiri mtu kwamba si muathirika kwa kumuangalia umbo na muonekano wake wa nje ila hivi sasa watu wanamuamko wa kuangalia afya za wenzi wao katika vituo vya afya mbali mbali.
Kama mtu akigundua yuko salama huwa mwangalifu zaidi na kama akijigundua ni muathirika hutumia dawa haraka iwezekanavyo.Hali hii ikiendelea virusi hivyo havitapata nafasi tena.

No comments: