Thursday, 17 July 2014

Ikulu ya Somalia yashambuliwa tena na Al Shabab


Wanamgambo wa kundi la kisomali la Al-Shabab washambulia Ikulu ya rais katika mji mkuu wa Mogadishu siku ya Jumanne magharibi ikiwa ni shambulio la pili mwaka huu dhidi ya ikulu hiyo.
Maafisa wa Usalama mjini Mogadishu wanasema hakuna ofisa wa serikali aliyejeruhiwa, lakini wanamgambo na walinzi ni miongoni mwa watu  walouliwa.
Mashahidi wanasema walisikia milipuko mikubwa na milio ya bunduki  kutoka Ikulu ya rais inayojulikana kwa jina la "Villa Somalia", wakati watu waalipokua wanajitayarisha kufuturu mnamo mwezi huu wa Ramadhan.
Mbunge Hussein Arab Isse ameiambia Sauti ya Amerika kwamba alikua ndani ya jengo la Ikulu wakati shambulio lilipotokea.
"Tulisikia mlipuko mkubwa na kulikuwepo na mapigano makali kati ya wanajeshi na watu hawa wa Al-Shabab na ilikua inafanyika nje ya dirisha langu."
Msemaji wa serikali Ridwan Haji ameiambia Idhaa ya Kisomali ya Sauti ya Amerika kwamba maafisa wote wa vyeo vya juu wako salama na wanajulikana mahala walipo.
"Rais Hassan sheikh Mohamoud, waziri mkuu na mawaziri wengine wote, wako salama  nilizungumza na waziri mkuu na mawaziri wengine na wote wako salama."
Waziri wa habari wa Somalia Mustaf Shiekh Ali anasema washambuliaji wanne wakiwa na bunduki ndani ya gari walijaribu kuingia kwa nguvu ndani ya uwanja wa Ikulu lakini walizuliwa katika kituo cha ukaguzi. Anasema washambulizi walilipua bomu ndani ya gari kabla ya kujaribu tena kuingia katika jengo hilo lenye ofisi za mawaziri kadhaa kwa kutumia nguvu na mashambulizi ya bunduki.
Waziri Sheikh Ali ameiambia amesema kwamba washambulizi watatu waliuliwa na dereva kujeruhiwa na anashikiliwa na maafisa wa usalama.
Mkuu wa polisi  Kasim Ahmed Roble anasema wanajeshi watatu wa serikali waliuliwa katika shambulio hilo.
Kundi la al shabab limeshadai kuwajibika na shambulio hilo.
Rais Mohamoud akilihutubia taifa Jumanne jioni alikanusha uvumi kwamba alikimbia kutoka Ikulu. Alisema magaidi wanaweza kueneza madai na vitisho vyao namna wanavyotaka, kwenye mtandao, lakini hawatofanikiwa kuwauwa na wale kuweza kuwazuia katika dhamira ya kulilinda taifa.
Afisa wa zamani wa serikali mjini Mogadishu anasema rais alikua anahudhuria sherehe wakati wa futari katika jengo lenye ulinzi mkali la uwanja wa ndege.
Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa Al-Shabab kujaribu kuushambulia uwanja wa Ikulu ambako kuna majengo ya serikali na makazi ya baadhi ya maafisa wa vyeo vya juu.
Katika shambulio la kabla, la mwezi Februarimjitoa mhanga aliendesha gari lililojaa milipuko na kulilipua kwenye mlango mkuu wa Ikulu na hapo tena kuzuka kwa mashambulio ya bunduki  na kusababisha vifo vya watu 14.

No comments: