Friday, 15 April 2016

Phiri:Wachezaji wangu wa viwango




Kocha Mkuu wa Mbeya  City Fc  Mmalawi Kinnah Phiri amesema  sasa ana uhakika  kuwa nyota wake wako kwenye kiwango kizuri  kufuatia  matokeo ya  ushindi wa jumla ya mabao 5  kwenye michezo miwili  iliyopita  kwenye  mfululizo  wa mechi za  Ligi Kuu ya Soka  Tanzania Bara inayoelekea  ukingoni hivi sasa. 
Phiri15
Kocha Kinnah Phiri
Phiri ameayasema hayo leo wakati akizungumza na mtandao wa Mbeya City fc.Com na kuweka wazi kuwa  ushindi wa 4-0 dhidi ya Coastal Union na  ule wa 1-0 dhidi ya Mgambo JKT mwishoni mwa juma lililopita umempa  imani kubwa kuwa wachezaji wake sasa  wameanza kuielewa vyema  falsafa yake hasa kwa kuweza kufanikisha ushindi bila  kuruhusu kufungwa bao katika michezo hiyo miwili.
"Tulianza  kucheza  kwa  mchezo wa kawaida  sasa  tumeongeza, tunacheza kwa spidi kubwa wachezaji wangu sasa  wanajiamini kwa kiwango kikubwa, tumefunga bao 5 bila kuruhusu kufungwa bao lolote, ni uhakika tosha kuwa kikosi changu sasa  kiko imara kwenye ulinzi," amesema na kuongeza.
"Pia  kiko vizuri kwenye ufungaji, kwa sasa  tuko kwenye mipango  mizito  kuhusina na mchezo ujao."
Kocha huyo aliyewahi  kuifundisha Timu ya Taifa ya Malawi alisema kuwa  mara baada ya kurejea  kutoka  jijini Tanga kwenye mchezo dhidi ya Mgambo JKT  alitoa siku chache za mapumziko kwa wachezaji wake na kuwataka  kujiandaa kwa mazoezi yatakayoanza  siku ya jumatatu tayari kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopangwa  kuchezwa  mwishoni  mwa mwezi huu.


"Baada ya kutoka Tanga, nilitoa mapumziko ya siku saba, vijana watarejea  jumatatu tayari kwa mazoezi  kabla ya kuivaa Mtibwa, nina  imani siku saba  zitatosha  kuwaweka sawa kwa ajili ya mchezo huo," amesema.
"Sifahamu sana  kuhusu timu hiyo ya Morogoro, kwenye ratiba  inaonyesha watacheza kesho  ninaweza kufika  kuwaona au  nitatumia  muda kuangalia mchezo wao kwenye TV, nataka kujua baadhi ya mambo muhimu ili nijiandae  vizuri kuweza kupata ushindi," amesem.

Saturday, 5 March 2016

TFF: Atuhusiki wala hatujatoa kibali cha michezo ya Betting


SHIRIKISHO la  Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema halihusiki na halijawahi kutoa kibali chochote cha kuhusisha  mashindano yake na michezo ya kubahatisha.
 Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto ameyasema hayo leo katika ofisi za TFF zilizopo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa Shirikisho limepokea kwa mshtuko taarifa za kuwepo makundi ya watu na makampuni wanaochezesha michezo ya kubahatisha inayohusu mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na kusimamiwa na TFF (betting).
“TFF inauthibitishia umma wa watanzania kuwa Shirikisho halihusiki wala halijawahi kutoa kibali chochote cha kuhusisha mashindano yake na michezo ya kubahatisha,” amesema Kizuguto.
 Moja ya jengo linalotoa huduma za mchezo wa kubahatisha (Betting)
Kizuguto amefafanua hatua zilizochukuliwa na TFF baada ya kubaini hilo, ikiwa ni pamoja na kuwaandikia barua wahusika ambao ni makampuni ya nje.
“Kwa kuwa baadhi ya wahusika wa matendo hayo ni makampuni ya nje ya nchi hivyo TFF imechukua hatua zifuatazo:
1.TFF imeandika barua kwenye Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa ili kupata mwongozo wa kisera na kisheria kuhusu haki na majukumu ya Shirika hilo  katika kudhibiti na kusimamia  jambo hilo.
2.TFF imeandika barua kwa kitengo cha sheria cha FIFA ili kupata mwongozo na ushauri wa namna ya kudhibiti makampuni ya nje yanayoshiriki mchezo huu.
TFF inawaomba wadau wa mpira wa miguu na washiriki wa michezo ya kubahatisha wajiepushe kushiriki michezo ya kubahatisha inayohushu michezo yote inayoandaliwa na TFF,” amesema Kizuguto.

Jamii Media yaitaka Mahakama Kuu kurekebisha vifungu vya sheria ya mtandao


Na Regina Mkonde
KAMPUNI ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com imefungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kesi Na. 9 ya mwaka 2016 la kuitaka Mahakama kurekebisha sheria ya makosa ya mtandao vifungu Na. 32 na 34
Hatua hiyo imefikiwa baada ya miezi mitatu iliyopita Kampuni hiyo kupata mashinikizo kutoka kwa Jeshi la Polisi (kwa njia ya barua rasmi) kuitaka itoe taarifa za baadhi ya wateja wanaoonekana kutoa taarifa zinazoibua ufisadi na ukwepaji kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa shauri hilo katika Mahakama Kuu iliyopo jijini dar es Salaam jana, Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media amesema kuna ulazima wa vifungu hivyo kuangaliwa upya kwa kuwa vinapelekea kuvunjwa kwa haki ya kulindwa uhuru wa utoaji maoni.
“Baada ya kupata mashinikizo takribani manne yanayoashiria kuwa haki ya watanzania watumiao mitandao ya kijamii hasa mtandao wa Jamii Forums inavunjwa, Jamii media imeshauriana na Wanasheria wake na kuona ni wakati wa kulinda haki ya wananchi,” alisema Melo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media Maxence Melo (Kushoto) akiwa kati ya moja ya mikutano na waandishi wa habari.

Melo alisema kuwa, lazima watailinda haki ya wananchi ya kupata taarifa na kulindwa kwa uhuru wao wa maoni na kujieleza inayolindwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ibara ya 18.
 “JamiiForums katika kuhakikisha inasimamia usiri(Privacy) wa wateja wake imekuwa ikihoji mashinikizo hayo yanazingatia sheria gani na kutaka kujua vifungu gani vya sheria ambavyo wadau hao wa mtandao wamevivunja,” alisema.
Alisema, hawakuwepewa majibu yoyote na Jeshi la Polisi badala yake kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama hawatatoa ushirkiano kwa Jeshi hilo.

Benedict Alex, Wakili wa Kampuni ya Victory Attoneys anasimamia Shauri hilo, alisema kuwa vifungu hivyo vinakinzana na Katiba ya nchi na kwamba ili iende sambamba na katiba haina budi kubadilishwa.

Thursday, 17 December 2015

Shirika la OXFAM lapania kuwezesha vijana

Shirika lisilo la kiserikali la OXFAM kwa kushirikiana na taasisi tano za vijana nchini(DARUSO,TYDC,YouthCAN,YOUNG FEMINIST FORUM na NGAO YOUTH ) limepania kuwainua vijana walio chini ya umri wa miaka 24 kiuchumi na kutimiza ndoto zao kupitia mradi wao wa MSAFARA.
Vijana wa Msafara wakielekea Ifakara
Hivi sasa mradi wa Msafara upo kwenye majaribio ambapo wameshafanya matamasha mawili Dar Es Salaam na Morogoro.Jijini Dar Es Salaam tamasha lilifanyika tarehe 4 disemba kwenye ukumbi wa Nkurumah, lilihudhuriwa na vijana zaidi ya 500 kutoka sehemu mbalimbali
vijana waliohudhuria tamasha la Msafara kwenye ukumbi wa Nkurumah,jijini Dsm
,na tamasha la mkoani Morogoro lilifanyika kwenye Uwanja wa Taifa uliopo Ifakara wilaya ya Kilombero tarehe 12 disemba mwaka huu.
Mradi wa Msafara unatarajiwa kuanza rasmi Januari mwakani,unatarajiwa kuzunguka Tanzania nzima na kuchagua vijana wenye vipaji,ndoto na mawazo yatakayobadilisha maisha yao na Taifa kiujumla.
Lengo la Msafara ni kuwawezesha vijana kuwa wabunifu,kuwahamasisha ili kuzifikia ndoto zao na kuwatengenezea mazingira rafiki yatakayo wawezesha wao kujiajiri wenyewe.
 Mwenyekiti wa Msafara Bw. James Isdore,aliwataka vijana kuitumia fursa hii ili kujitengenezea mazingira mazuri ya wao kujiajiri na kuwezeshwa kiuchumi.
Mwenyekiti wa Msafara(wa pili kutoka kushoto) James Isdore akiongea na Waandishi wa Habari Dsm

"Vijana inabidi wajifunze kuzitumia fursa kama hizi,mradi wa Msafara una lengo la kuweka ubunifu wa vijana wazi ili kuwavutia wengine waweze kufanya zaidi na kuimarisha ubunifu wao,pia tunahamasisha vijana kuchukua hatua na kufanya zaidi basada ya kujifunza kutoka kwa wenzao pamoja na kuziibua changamoto za mafanikio ya kimaisha na jinsi ya kukabiliana nazo." Alisema Isdore     

Saturday, 11 October 2014

Mlipuko wa Ebola waipa hofu nchi ya Morocco

Vyombo vya habari nchini Morocco vinasema kuwa serikali ya taifa hilo imeomba kinyang'anyiro cha kuwania kombe la klabu bingwa barani Afrika cha mwaka ujao kuahirishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa ebola.
Maiti ya Mgonjwa wa Ebola ikienda kuhifadhiwa na wahudumu
Hatua hiyo iliafikiwa kutokana na pendekezo la wizara ya afya ambayo inataka kuyazuia mataifa ambayo yameathiriwa na ugonjwa huo.
Maafisa nchini Moroco watafanya mazungumzo kuhusu ombi hilo na waandalizi wake ambacho ni chama cha kandanda barani afrika CAF wiki ijayo.
Mechi za kufuzu zinazoshirikisha nchi mbili ambazo zimeathiriwa na ugonjwa wa ebola ambazo ni Guinea na Liberia tayari zimehamishwa ikiwamo mechi ambayo ilitarajiwa kuchezwa leo .

USA yawakagua raia wanaotoka mataifa yaliyoshambuliwa na Ebola

Mpango mpya wa ukaguzi umetangazwa nchini Marekani kujaribu kupunguza kuwasili kwa wageni walio na ugonjwa wa Ebola.
Wasafari ambao wanawasili mjini New York kutoka nchi tatu zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa Ebola Magharibi mwa Afrika kama vile Guinea, Liberia na Sierra Leone watafanyiwa ukaguzi.
Programu hiyo pia inatarajiwa kupelekwa kwenye viwanja vyengine majuma yajayo.
Nchini Uhispania takriban watu 17 wametengwa baada ya wao kukaribiana na muuguzi ambaye sasa ni mgonjwa sana hospitalini.
Morocco nayo inasema kuwa inataka kuahirisha mashindano ya kuwania klabu bingwa barani Afrika kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola.
Mmoja kati ya askari wanaokagua raia wanaotoka nchi zilizo athiriwa na Ebola
Tangu ugonjwa huo uibuke magharibi mwa Afrika umesababisha vifo vya maelfu ya Waafrika na kusababisha watoto yatima na wajane kuongeza.
Aidha,benki kuu ya dunia hivi karibu katika mkutano wa nne uliohusisha nchi za barani Afrika uliofanyika Washington DC Marekani ilisema kuwa kuna uwezekano wa mataifa yaliyoathiriwa na janga hili yakashuka kiuchumi na kupoteza idadi kubwa ya watu.

Boko Haram lawaachilia mateka 27



Rais wa Cameroon amesema kuwa mateka 27 wakiwemo raia 10 wa Uchina wameachiliwa na kundi la wanamgambo wa Boko Haram.
Wanamgambo wa kundi la Boko Haram
Raia hao wa China walitekwa nyara mwezi mei wakati kampuni moja ya China ilipovamiwa karibu na mpaka wa Nigeria.
Wengine walioachiliwa ni pamoja na mke wa naibu waziri mkuu nchini Cameroon aliyetekwa nyara mwezi Julai.
Haijulikani iwapo fidia ililipwa.
Boko haramu wameeneza mashambulizi kutoka nchini Nigeria kwenda kaskazini magharibi mwa Cameroon.